Tuesday, April 21, 2009

WALEMAVU NI WENZETU TUWAJALI

SEMINA YA SIKU NNE YA WATU WENYE ULEMAVU ILIYOFANYIKA KIBAHA –PWANI KUANZIA TAR 6-9 APRIL MWAKA HUU.

Mimi ni mmoja wa watu ambaye nilishiriki Semina ya Siku nne ya Haki za Watu Wenye Ulemavu iliyoandaliwa na Taasisi ya Cheshire ambapo semina hiyo ilifanyika Wilayani Kibaha Mkoani Pwani katika chuo cha maendeleo ya Jamii kilichopo Tumbi.

Katika Semina hiyo ambayo ilishirikisha watu mbalimbali wakiwemo Watu wenye Ulemavu -WWU ,Madiwani, waandishi wa Habari za watu wenye Ulemavu kutoka mtandao wa wanahabari za WWU –MWAKU pamoja na watendaji mbalimbali kutoka Serikalini.

Semini hiyo ambayo ilikuwa ya aina yake iliweza kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mada zinazohusu masuala ya watu wenye ulemavu.

Watu mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu walishiriki katika kutoa mada ambapo kulikuwa na changamoto mbalimbali.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ya siku nne ni Haki za Watu Wenye Ulemavu katika mtanzamo wa Mikakati ya Kimataifa Juu ya Haki za Binadamu, Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu, na Changamoto za Watu Wenye Ulemavu Dhidi ya Umaskini na Misingi ya Haki za Binadanu .

Nyingine ni pamoja na Ushiriki wa Watu Wenye Ulemavu katika Sera na Mikakati yake na Ushawishi na Utetezi kwa Watu wenye Ulemavu.

Mara baada ya kuwasilishwa kwa mada hizo washiriki walijadili na kuchangia mada hizo ambapo kwa watu ambao tulikuwa na uelewa mdogo kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu tulifaidika na kuelimika.

Kutokana na mada hizo binafsi nikiwa mwandishi wa habari mambo mengi kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu nilikuwa siyafahamu vizuri kupitia semina hiyo nimeweza kufahamu na kujifunza mambo mengi kuhusu WWU.

Siku nne kwa upande wangu zilikuwa za mafunzo tosha kwa kuwa katika kazi yangu ya uandishi inahitaji uelewa wa kutosha katika masuala mbalimbali ili kuelimisha jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu.


Katika Semina hiyo masuala mbalimbali yalijitokeza ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu kuulaumu uongozi wa mkoa wa Pwani kutotoa ushirikiano kwa jamii ya watu wenye Ulemavu kitu ambacho WWU kuona wanatengwa na Uongozi wa Mkoa.

Serikali ina jukumu kubwa la kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki sawa kwa kuhakikisha sheria na sera zilizopo zinatimizwa kwa kuwa wamekuwa wakitengwa katika sehemu mbalimbali.

Kama ni sheria tumeziweka wenyewe kama ni sera tumezitunga wenyewe kwa hiyo hakuna sababu ya kutozisimamia ili WWU waweze kupata haki zao kama ambavyo watu wasio na ulemavu wamekuwa wakipata.

Lakini hatuwezi kutimiza hayo yote iwapo jamii ya watu wenye ulemavu yenyewe haitasimama na kutetea haki zao wenyewe wala hawatajijali wenyewe hivyo ni vema WWU wakawa mfano katika kuhakikisha wanapigania haki zao wenyewe kwa kuwa wana haki sawa kama watu wasio na ulemavu.

Kama watanzania tunatakiwa kuona jamii ya watu wenye ulemavu kuwa ni wenzetu wanahitaji mapenzi kwa kuwa na wana haki sawa kama watu wasio na Ulemavu.

Lakini kubwa zaidi ni kukumbuka kuwa sisi sote ni walemavu watarajiwa hivyo hatuna sababu ya kuwatenga au kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu.

Ni mengi nimeweza kujifunza katika semina hiyo na jinsi ya kuandika habari ambazo zitasaidia kuwaelimisha watanzania kuhusu masuala na haki za watu wenye ulemavu.